MATUKIO
yanayohusishwa na imani za kishirikina ya watu kujeruhiwa,kuuawa na
fisi na kisha kugombea nyama yake na kwenda kuipika kwa ajili ya kitoweo
yamezidi kushika kasi kwenye mkoa huu wa Geita.
Juzi,Fisi
mwingine mwenye kichaa amevamia makazi ya watu na kung’ata watu watano
sehemu mbalimbali ya miili yao wilayani Bukombe mkoani Geita.
Mganga
mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Bukombe Dk Tenesigwa amethibitisha
kupokea kwa majeruhi hao kutoka Kijiji cha Ililika Wilayani humo.
Amewataja majeruhi hao kuwa ni Hamis Mpendakula,Mateso Manyanda Bugolo,Manyanda Bugolo,Dalali Selemani,na Mhoja Deusi.
Amefafanua
kuwa kati ya hao,Hamis Mpendakula amejeruhiwa vibaya sana na kufunuliwa
ngozi ya kichwa pamoja na uso na kufanya fuvu la kichwa kubaki wazi na
fuvu hilo limepasuka.
Amesema
wengine wamevunjwa vunjwa vidole vyao na kujeruhiwa baadhi ya viungo
vya miili yao na wamewapa rufaa ya kwenda hospitali ya Bugando kwa
matibabu zaidi.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ,mkuu wa Wilaya
ya Bukombe Amani Mwenegoha ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya hiyo
kuchukua hatua ya kujihadhari na kuimarisha ulinzi wa Jadi(sungusungu).
Mwenegoha
amesisitiza kuwa,kuanzia sasa kila Kijiji kwenye Wilaya yake kinatakiwa
kuimarisha ulinzi wa jadi na kwa kuwa fisi aliyefanya kitendo hicho
ametajwa kuwa na kichaa aliwataka wananchi kuacha kutembea hovyo hasa
nyakati za usiku hadi hapo fisi huyo atakapopatikana na kuuawa.
‘’Nina
imani huyu Fisi atapatikana haraka ipasavyo na ninawaomba wananchi
iwapo watasikia kelele kwenye mazizi yao ya ng’ombe nyakati za usiku
wajue ndiye fisi huyo na wapige mayowe ili watu wengi wakusanyike na
kumzingira hadi kumuua’’alisema Mwenegoha.
Mkuu
wa wilaya huyo tayari amewaagiza maafisa wa wanyamapori kwenye Wilaya
yake kufanya msako usiku na mchana hadi hapo watakapohakikisha fisi huyo
ameuawa kwa kuwa anatishia uhai wa watu wa Wilaya hiyo na maeneo ya
jirani.
Mwishoni mwa wiki iliyopita baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ihayabuyaga,kata ya kalangalala Wilayani Geita waliamua kugawana
nyama ya fisi aliyegongwa na gari usiku katika barabara kuu ya Mwanza
Kagera wakati akikatiza mitaa ya mji huo jirani na ilipo gereji ya
mabasi ya Lushanga.
Mbali
na hilo,matukio haya yamekuwa yakitokea kwa wingi wilayani Geita
yakiwemo ya watu kushambuliwa na mnyama huyo aina ya fisi hususani
watoto chini ya Umri wa miaka Mitano na hivi karibuni fisi mwingine
alivamia mtaa na kuanza kushambulia watu hovyo kwa kuwauma kabla ya
polisi kufika eneo hilo na kumuua kwa risasi kisha kutoa mwanya kwa
wananchi kugombea nyama yake na kuifanya kitoweo.
Tukio
hilo la kusitaajabisha na ambalo liliacha maswali mengi,lilitokea
mwishoni mwa mwezi Juni,majira ya saa 9 alasiri katika mtaa wa
Kabahelele,Kata ya Katoro Wilaya ya Geita Mkoani Geita.
Wakati
polisi wanafika eneo hilo,tayari Fisi huyo alikuwa amefanya madhara kwa
watu watatu ambao waling’atwa sehemu za miguuni na midomoni hali
iliyowalazimu polisi kutawanya watu kisha walifanikiwa kumuua fisi huyo
kwa kumpiga risasi zaidi ya mbili.
Waliojeruhiwa
na Fisi katika tukio hilo,walikuwa ni Bugamba Zumbe(21),Peter Francis
(32),na mwingine ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja wote
wakazi wa mtaa huo wa Kabahelele.
Baada
ya Fisi huyo kuuawa,baadhi ya wananchi wa eneo hilo nusura wauane kwa
kukatana visu wakigombea nyama ya mnyama huyo na walipohojiwa na
Malunde1 blog kuhusu nini sababu za kugombea nyama hiyo walidai inaliwa
na kwamba ikipikwa vizuri inazidi hata ile ya ng’ombe.
Tukio
jingine ni la Masumbuko John(35) mkazi wa Nyabulanda Tarafa ya
Nyang’hwale Wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita aliyeuawa kwa kushambuliwa
na Fisi na kuliwa,sehemu za Tumbo,mguu mmoja ukiwa umebaki mfupa na ule
wa kulia pamoja sehemu za usoni kichwani na kifuani.
Ofisa
Misitu na Maliasili wa Wilaya ya Geita Kasika Gamba amedai chanzo cha
Fisi kushambulia watu,na kuonekana sehemu za mjini ni kutokana na
uharibifu wa mazingira katika Hifadhi za Mistu hali ambayo imesababisha
wanyama hao kuzagaa kwenye makazi ya watu kutokana na kukosa sehemu ya
kijihifadhi na kujipatia chakula.
Daktari
wa Mifugo wa Wilaya ya Geita Thobias Kiputa, amewataka wananchi kuepuka
kula hovyo nyama za wanyama ambao siyo wanyama(Meat Animals)ambao ni
wala nyama kama Fisi ambao hawajakaguliwa kwa alichodai kula nyama ya
wanyama wala nyama kama fisi,ambao hawajakaguliwa wanaweza kuwa na
magonjwa mbalimbali yanayoweza kuwasababishia madhara ya afya.
Na Victor Bariety-Malunde1 blog-Geita
No comments:
Post a Comment