Shirika la misaada la Madaktari
wasiokuwa na mipaka MSF, limeshutumu vikali umoja wa mataifa kutokana na
hali duni ya maisha katika mojawapo ya kambi zake kaskazini mwa Sudan
Kusini.
MSF inasema zaidi ya wakimbizi elfu arobaine waliofurushwa makwao mjini Bentiu wanaishi katika mazingira ambayo maji ya mafuriko yamechanganyika na maji taka.
Katika taarifa yake , shirika hilo limesema hali duni katika kambi hiyo ni ukiukaji wa haki za hadhi ya binadamu. Sasa MSF imetaka Umoja wa Mataifa kuwahamisha walioathirika zaidi na mafuriko hayo.
Umoja wa Mataifa haujajibu madai hayo hadi kufikia sasa.
Maelfu ya wenyeji ambao ni wakimbizi wa ndani kwa ndani mwa taifa hilo wametafuta hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa katika mji huo ulioko kwenye jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Unity.
Na baada ya msimu wa mvua kuanza, MSF inasema hali ngumu katika kambi hiyo sasa imekuwa hata mbaya zaidi.
Picha kutoka angani zinaonyesha sehemu kadhaa za kambi hiyo zikiwa zimesombwa na maji.
Aidha picha nyingine zinaonyesha watoto na akina mama wakitembea katika maji mengi ya mafuriko.
Wengine wengi walilala wakiwa wamesimama huku wakiwashikilia watoto wachanga mikononi.
Shirika hilo sasa linataka Umoja wa Mataifa kutumia ardhi kavu kando na kambi hiyo kupeana makao mapya kwa familia zilizoathirika zaidi na mafuriko.
Mapigano kati ya waasi na vikosi vya serikali yamewafurusha zaidi ya watu milioni moja unusu kutoka mkwao.
VIA :BBC SWAHILI.
No comments:
Post a Comment