Friday, August 29, 2014

MGONJWA ALIYEHISIWA KUFA KWA EBOLA GEITA AZUA MJADALA, SAMPULI ZATUMWA WIZARA YA AFYA KWA UCHUNGUZI ZAIDI.

Utata umegubika kifo cha Bertha Boniface (25) ambaye amefia Hospitali ya Wilaya Geita, kutokana na uvumi kuwa kifo chake kinatokana na ugonjwa wa ebola. Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na uongozi wa wilaya hiyo.

Viongozi hao wamedai hakuna mgonjwa aliyekufa kwa maradhi hayo na wala ugonjwa huo haupo. Umesema Bertha alikuwa akihisiwa kuwa na dalili za ebola.
Akizungumzia uvumi huo, mganga mfawidhi wa Wilaya ya Geita, Dk Adam Sijaona alisema siku kumi zilizopita walimpokea mgonjwa kutoka mji mdogo wa Katoro ambaye alikuwa akitapika, kuharisha damu na kutokwa damu mdomoni na puani.
“Kutokana na hali hiyo, tuliamua kuchukua tahadhari. Tulimlaza kwenye chumba maalumu ili kumfanyia uchunguzi wa kina,” alisema Dk Sijaona.
“Tayari tumetuma sampuli Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa uchunguzi zaidi, kwa sababu hospitali yetu haina vifaa vya kupima ebola. Tumekaa na mgonjwa huyo lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia Jumatano.

 Tunasubiri majibu ya mwisho, lakini uchunguzi wa awali unaonyesha inaweza isiwe ebola, hivyo watu wasiwe na hofu. Ugonjwa huo haujaingia mkoani kwetu.”
Hata hivyo, uongozi wa hospitali hiyo ulikataa kukabidhi mwili wa marehemu kwa familia kwa ajili ya maziko na badala yake ulizikwa na Serikali.
Dk Sijaona alitetea uamuzi huo wa Serikali kuzika akisema ulitokana na kutojua sababu za kifo chake.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Geita, Dk Noel Makuza alisema Bertha awali alikuwa akisumbuliwa na malaria, lakini siku tatu baadaye alianza kuharisha na kutapika damu nyingi.
“Inawezekana pia alikuwa na vidonda vya tumbo, hata hivyo katika vipimo tulibaini pia alikuwa na homa kali ambayo kitaalamu inajulikana kama haemorge fever inayoendana na ile ya dengue au ya bonde la ufa,” alisema.
“Lakini pia tulipokuwa tukimchoma sindano, damu ilikuwa inaganda na eneo husika linakuwa jeusi. Kwa sababu ya utata huo tuliamua kupeleka sampuli wizarani kwa ajili ya vipimo. Nina imani kuwa wiki hii majibu yatapatikana.”
Alisema kitaalamu iwapo ugonjwa huo ni ebola, ndugu wa Bertha waliokuwa wakimhudumia wataanza kuumwa au kuonyesha dalili baada ya siku nane.
Jumatano wiki hii ndugu wa Bertha walikwenda Hospitali ya Wilaya ya Geita wakitaka kuchukua maiti kwa ajili ya maziko, lakini uongozi wa hospitali ulikataa kwa sababu za kiafya.

Waliomba tena waruhusiwe hata kutoa heshima za mwisho, pia walikataliwa.
 Story na Salum Maige,Geita.

No comments:

Post a Comment