Vyumba 20 vya bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya African
Muslim, iliyoko Kata ya Kaloleni, Manispaa ya Moshi, mkoani
Kilimanjaro, vimeteketea kwa moto.
Moto huo ambao ulizuka juzi saa 1:45 jioni na kuwaka kwa zaidi ya saa
tano, ulianzia katika choo cha shule hiyo, jirani na Bweni la Makka
kabla ya kuruka kwenye chumba cha jirani na kusambaa kwenye vyumba 20
vilivyoko katika bweni hilo.
Akizungumza toka eneo la tukio, Mkurugenzi wa Shule
hiyo, Ali Adam Ali, alisema moto huo ambao hadi sasa chanzo chake
hakijajulikana japo inadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme, umesababisha
hasara kubwa kwa wanafunzi zaidi ya 96 wa kidato cha nne wanaotumia
bweni hilo.
“Moto huu ulianza majira ya saa mbili kasoro, wanafunzi walikuwa
wanajiandaa kuingia katika swala ya Isha, mmoja wa wanafunzi alihisi
harufu ya moto na kuwajuza wenzie, baadae wakaanza kuhangaika kutafuta
ni wapi chanzo chake kilipo, waligundua kuwa ulianzia chooni, ghafla
ukasambaa katika vyumba vingine vya ghorofani kupitia chumba cha jirani
na choo,” alisema Ali.
Alisema hakukuwa na madhara makubwa yaliyotokana na moto huo kutokana
na wanafunzi wengi kuwa likizo, na kwamba ni wanafunzi wa kidato cha
nne na kidato cha pili tu ndio walioathirika na moto huo.
“Hakuna majeraha makubwa kutokana na tahadhari ya kiusalama
tuliyochukua kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali ya Mtaa, wanafunzi
walijitahidi kuondoa vitu vyao, vitanda na mabegi ya baadhi yao
vimeungua katika moto, wanafunzi wanne walipoteza fahamu, tuliwakimbiza
hospitali na sasa wanaendelea vizuri,” alisema Ali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa, Kaimu Mkuu wa Mkoa
wa Kilimanjaro, Dkt. Ibrahim Msengi, aliuagiza uongozi wa shule hiyo
kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa na Ofisa Elimu wa mkoa
kufanya tathimini ya hasara iliyotokana na moto huo.
Wakati huo huo, Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Kilimanjaro, Estomih
Makyara amemtaka mkurugenzi wa shule hiyo kutoa wiki moja ya mapumziko
kwa wanafunzi walioathirika na moto huo, isipokuwa wanafunzi wa darasa
la saba wanaoendelea na mitihani wataendelea kama kawaida.
No comments:
Post a Comment