Monday, October 6, 2014

MWALIMU WA SEKONDARI HUKO RUKWA ATUNDIKWA MIMBA NA MWANAFUNZI WAKE WA KIDATO CHA PILI.

WAKATI ikiwa imezoeleka kuwa baadhi ya walimu wa kiume huwarubuni wanafunzi wao wa kike na hata kuwaharibia kabisa ndoto zao za kielimu kutokana na kuwapa ujauzito, hali imekuwa tofauti mkoani Rukwa ambako mwanafunzi wa Kidato cha Pili anadaiwa kumzalisha mwalimu wake.



 
Mwanafunzi huyo aliyemzalisha mwalimu wake ana umri wa miaka 17, wakati mwalimu huyo anayefundisha katika Shule ya Sekondari ya Umma ya Nkasi, iliyopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, Rukwa, ana umri wa miaka 25.
 
Tukio hilo linalotajwa kuwa la kwanza kutokea wilayani hapa, limekuwa gumzo kubwa kwa wakazi wa Nkasi na wilaya jirani.
 
Hata hivyo, kwa wanafunzi, wamekuwa wakimpongeza mwenzao kwa kujaliwa kupata mtoto katika umri wake huo mdogo, huku mzazi mwenzake akiwa na uhakika wa maisha kutokana na kuwa ni mtumishi serikalini.
 
Imeelezwa kuwa licha ya tukio hilo, mwalimu huyo aliyezaa na mwanafunzi wake bado anaendelea na masomo shuleni hapo, huku `mzazi’ huyo wa kiume akifundishwa na mzazi mwenzake.
 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Namanyere hivi karibuni, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nkasi mjini Namanyere ambayo ni ya mchanganyiko ya umma, Amiamie Nanga alisema mwalimu huyo alianza kazi shuleni hapo ikiwa ni mara yake ya kwanza kufundisha baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu chuoni.
 
“Yameshatokea, lakini haileti picha nzuri sana, lakini mimi nina uzoefu mkubwa na wakazi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika, kwao si ajabu kuwa na uhusiano na watu waliowazidi umri, iwe kwa mtoto wa kike au wa kiume, wote ni sawa tu…
 
“Lakini katika kisa hiki, inaonesha walimu sasa wanapoteza haiba ya ualimu. Hii kazi ina miiko na maadili yake …kwa mwalimu huyu hii ni ajira yake ya kwanza, nikimaanisha ni kituo chake cha kwanza cha kazi tangu ahitimu masomo yake…” alisema.
 
 Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema hakuna kosa kwa mwalimu huyo wa kike kwa kuwa tayari ni mtu mzima.
 
“Isitoshe katika kisa hiki ni nadra kumpata mlalamikaji … Mwalimu mwenyewe huyu wa kike hawezi kuwa tayari kujidhalilisha kuwa amebakwa, yalikuwa maamuzi yake.”
 
Aliongeza kuwa, kwa mwalimu huyo kupata ujauzito wa mwanafunzi wake hakuwezi kuathiri ajira yake, tofauti na mwalimu wa kiume akimpatia ujauzito mwanafunzi wake wa kike ambaye huathirika kwa kukatisha masomo.
 
Jitihada za kumpata mwalimu huyo wa kike na mwanafunzi huyo zimegonga mwamba baada ya watu wao wa karibu kumweleza  mwandishi  kuwa hawako tayari kuuzungumzia mkasa huo.
 
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa masharti ya kutoandikwa majina yao  kwa hofu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu shuleni hapo, pamoja na kukiri kutambua uhusiano baina ya mwanafunzi mwenzao na mwalimu wao, lakini walisema hivi sasa mwalimu huyo amesitisha uhusiano na mwenzao na kuanzisha uhusiano mpya na mwalimu mwenzao.
 
Walisema pamoja na mambo mengine ni kama mwanafunzi mwenzao ameathirika kisaikolojia baada ya ‘kupinduliwa’ na mwalimu wake wa kiume ambaye kwa sasa ndiye baba mlezi wa mtoto.
 
“Huyu mwalimu wa kike sisi sasa tunamwita shemeji yetu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwenzetu… penzi lao lilikolea hadi sasa ameweza kumzalia mtoto huyo…, lakini kwa sasa inavyoelezwa ni kwamba penzi limehamia kwa mwalimu mwenzake,“ alisema mmoja wao.
 
Baadhi ya watu wa karibu na mwanafunzi huyo wanakiri kuwa mwanafunzi huyo hana uwezo wa kifedha kumudu kumpatia malezi stahiki mtoto wake huyo, hivyo hata mzazi mwenzake alipoanza uhusiano na mwalimu mwenzake hakuwa na jinsi, bali kukubaliana na matokeo.
 
“Usiniandike jina, sisi tunashauri mwalimu huyo wa kike na mpenzi wake huyo wa kiume ambaye ni mwalimu mwenzake wahamishiwe shule nyingine kwa sababu kama kioo katika jamii wameteleza kwa kiasi kikubwa na watashindwa kuwajenga na kuwalea wanafunzi wao kimaadili.
 
“Isitoshe tunajiuliza sheria hapa inasemaje maana kama angekuwa ni mwalimu wa kiume amempatia mwanafunzi wake wa kike ujauzito angeshitakiwa na kufikishwa mahakamani na pengine kuhukumiwa kifungo kisichopungua miaka 30 jela, sasa kwa hili sheria inasemaje?” Alihoji.
 
Baadhi ya wazazi mkoani hapa waliohojiwa na mwandishi kwa nyakati tofauti wameelezea kushangazwa na tukio hilo, na hasa kwa jinsi mwalimu alivyoshindwa kujizuia `kujiachia’ kimapenzi kwa mwanafunzi wake.

Credit: Habarileo
 

No comments:

Post a Comment