Tuesday, April 29, 2014

MZAZI AMTOA MWANAYE CHUMBA CHA MTIHANI NA BAKOLA KISA NI MTOTO



MZAZI  mmoja  aliyejulikana kwa jina la  Tilu Bushi mkazi wa kata ya Mwawaza manispaa ya Shinyanga ,amemtoa  mtoto wake wa darasa la saba  kwenye chumba cha kufanyia mtihani wa Moko akiwa na fimbo mkononi  na kumtaka arudi nyumbani kulea mtoto.


Mzazi huyo alifanya tukio hilo juzi  wakati mtoto wake Magreth  Tilu anayesoma shule ya msingi Bugimbagu akiendelea kufanya  mtihani huo, ndipo aliamuwa kuchukuwa maamuzi hayo  na kusababisha  mwanafunzi  huyo  kushindwa  kufanya mtihani wake vizuri .

Kufuatia tukio hilo ambalo lilitokea juzi  majira ya saa tatu asubuhi shuleni hapo,  walitoa taarifa kwa jeshi la polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe zaidi,kutokana na kitendo cha kumnyima haki yake ya msingi mtoto Magreth ya kupata elimu,ambapo  baada ya taarifa kutolewa  mzazi huyo alikimbi na kutokomea kusikojulikana.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Evarist Mangalla alisema tukio hilo lilitokea wakati  mwanafunzi huyo akiwa anafanya mtihani wa moko wa darasa la saba,ambapo mzazi wake alifika ghafula na kuingia darasani kisha kumtaka  binti yake arudi nyumbani kulea mtoto ambaye haijafahamika kama ni wake au wa ndugu.

Kamanda Mangalla alisema jeshi la polisi linaendelea kumtafuta mzazi huyo afikishwe kwenye vyombo vya sheria  kutokana na tuhuma inayomkabili .

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga  Annarose  Nyamubi  alisikitishwa  kwa  kitendo  hicho alichokifanya mzazi huyo  kwani kinadhoofisha maendeleo ya elimu  kwa watoto wa kike katika wilaya na mkoa kwa ujumla na kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao  na wengine kukatisha masomo.

Nyamubi alisema mzazi huyo anatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo pamoja na kukumbushwa  majukumu yake katika kuhakikisha mtoto anapata elimu bila kubaguliwa kwani wote wanahaki sawa.


No comments:

Post a Comment