Nyumba inayosadikiwa kuwa inamisukule ambayo ilikuwa imefugwa na ajuza Nyanzila Mbasu(65) katika kijiji cha Ilebelebe wilaya ya Kishapu,Shinyanga.
Pata habari zaidi hapa.
MAMIA ya wananchi wa kijiji cha Ilebelebe kata ya Itilima wilaya ya
Kishapu mkoa wa Shinyanga wamefurika kushuhudia tukio la kijana mmoja
anayesadikiwa kuwa ni msukule, ambaye alionekana jirani na nyumba ya
kikongwe mmoja aliyefariki dunia mei 26 mwaka huu kwa kukatwakatwa
mapanga kwa tuhuma za ushirikina na kudai kuwa alikuwa anahifadhiwa na ajuza huyo.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku moja baada ya Ajuza aliyejulikana kwa jina la Nyanzala Mbasu (65) kuvamiwa na watu
wasiojulikana na kumcharanga mapanga nyumbani kwake kisha kutokomea
kusikojulikana ,ambapo siku ya mazishi yake yaliyofanyika juzi ndipo
kijana huyo alikutwa na wanachi nyuma ya nyumba hiyo saa tatu usiku
akizunguka na kusema kaamua kutoka nje baada ya kukosa chakula.
Kijana
huyo anayesadikiwa kuwa ni msukule anajulikana kwa jina la Ndaki Samola
ambaye alidai anatoka kijiji cha Ubale kata ya Samuye wilaya ya
Shinyanga,huku akizungumza kwa shida alisema alifika kijijini humo kwa
ajili ya kuoa, bila ya kufafanua ni kipindi gani amekaa na kwamba
alikuwa akiishi kwenye nyumba ya bati ya ajuza huyo na wenzake
wawili.
Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Ilebelebe Thomas Nkindo
alisema tukio hilo limewashangaza kwani kijana huyo hajawahi kuonekana
kijijini humo hata siku moja ,hali ambayo imewapa wasiwasi wananchi
kutokana na maneno aliyoeleza kwamba alikuwa kwenye nyumba ya ajuza
huyo ambayo imefungwa kwa muda mrefu na haitumiki. Alisema baada ya
kumuhoji sungusungu alidai kuwa kilichomtoa ndani ni njaa na kwamba
kawaancha wenzake wawili mmoja akiwa ni mwanamke ambao walikuwa wanakaa
pamoja nayeye, alikuja kwa ajili ya kuoa na kufikishiwa kwenye nyumba
hiyo ya tope ambayo imeezekwa kwa bati iliyokuwa ikimilikiwa na
marehemu.
Afisa mtendaji wa kijiji hicho Emmanuel Asili alisema
marehemu Mbasu kabla ya kufikwa na mauti siku hiyo ya tukio asubuhi
alikuwa amealika wanawake, ambao walifanya kazi ya kumsaidia kukata
mapalage ya viazi (maarufu kama michembe) ndipo usiku huo huo alivamiwa
na kuuawa majira ya saa 1.30 wakati akimpatia mbwa wake chakula.
“Kilichotushitua
zaidi huyo kijana Ndaki alikuwa anuka harufu ya nyama wakati tunamuona
na ukizingatia mchana kwenye mji huo ulipokuwa msiba walikuwa wamechinja
mbuzi,moja kwa moja wananchi walimtilia mashaka inawezekana akawa ni
msukule kwa kulinganisha na maelezo yake “alisema Asili.
Kutokana
na mashaka hayo waliamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi huku kijana
huyo akiwa amehifadhiwa kwa muda katika ofisi ya afisa mtendaji wa
kijiji kwa uangalizi zaidi,mara baada ya askari kufika eneo la tukio
walizungumza na wananchi na kuamuru mlango wa nyumba hiyo uvunjwe ili
kuona kilichomo ndani na kuiondoa wasiwasi jamii ambapo walikuta bati
lililochakaa,beseni na ndoo.
Akizungumza na wananchi mkuu wa
kituo cha polisi wilaya ya Kishapu ASP Samwel Kijenga aliwataka kutoa
ushirikiano ili kuwabaini watu waliosababisha mauaji hayo ya
kinyama,ambapo alisema wataendelea kufanya upelelezi na kwamba waondowe
wasiwasi nyumba waliyokuwa wakihofia wameangalia hakuna kitu hivyo
waendelee na shughuli za maendeleo.
Hata hivyo wakati kijana huyo
akiwa tayari amepandishwa ndani ya gari la polisi kwa ajili ya
kupelekwa kufanyiwa uchunguzi kama anamatatizo ya akili,alitokea baba
mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Nyalali Chaba na kudadi kuwa
anamfahamu ni mdogo wake anasumbuliwa na tatizo la akili .
Kamanda
wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Evarist Mangalla amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo la mauaji ya ajuza wa miaka (65) na tayari watu wanne
wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi wakati wakiendelea na
upelelezi.
|
No comments:
Post a Comment