MIFUKO ya hifadhi ya jamii nchini imetahadharishwa kuacha
kufanya kazi kwa kutapeli watumishi wapya wa serikali hususani waajiriwa wapya
kwa kutoa fomu ambazo zimeshajazwa bila kutoa ushauri mzuri, hali ambayo inasababisha baada ya muda
wateja wao kujutia kujiunga na mifuko hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa
jana na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi kwenye semina ya elimu juu
ya hifadhi ya jamii kwa viongozi wa serikali mkoa wa Shinyanga,ambapo alisema
baadhi ya mifuko haifanyi kazi zake kwa uwazi
hivyo kuwatapeli watumishi hasa waajiriwa wapya ambao wanakuwa
hawaifahamu vizuri.
Mkuu wa wilaya aliitaka mifuko hiyo kufanyakazi zake kwa
uwazi na kutoa huduma iliyobora kwa wateja wao ili kuwahamasha watumishi
wengine kutoka serikalini,mashirika,taasisi na watu binafsi kujiunga ili
kujiwekea akiba ya uzeeni pamoja na mafao mengine ukiwemo uzazi na matibabu .
“ Inaumiza pale ambapo unawekeza baada ya miaka mitano
halafu kinafanana na mtu aliyewekeza leo wakati gharama za maisha zinapanda
kila kukicha,ninawaomba ndugu zangu mnaosimamia mifuko hii kwenda na mabadiliko
ya hali halisi iliyopo”alisema Nyamubi.
Nyamubi alisema mfuko wa hifadhi ya jamii(NSSF) umekuwa
ukilalamikiwa na watumishi wengi kwa kushindwa kuboresha huduma zake, hali hiyo
inaweza kusababisha kukosa wananchama na malengo yao kutofikiwa na kutolea
mfano wakati wa mei mosi mabango mengi yalikuwa yakiulenga mfuko huo kwa
kuumiza watumishi katika mafao.
Semina hiyo ya siku moja iliandaliwa na mamlaka ya usimamizi
wa sekta ya hifadhi ya jamii (SSRA)alisema mifuko hiyo inatija kubwa iwapo jamii itaitumia vizuri
katika kujiletea maendeleo na kuweka akiba ya uzeeni,ambapo yote hayo
yatafanikiwa kwa kufanyakazi kwa uwazi na kuboresha huduma wanazozitoa .
Kwa upande wake mwezeshaji wa semina hiyo kutoka (SSRA) Dar
es salaam Mohamed Nyasama,alisema mpaka sasa ni 4.5 ya watanzania wote ndiyo
wamejiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii,idadi ambayo bado iko chini na
kuwataka watanzania kubadilika na kuwekeza kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii
kwa kuwa ni mkombozi wa kweli.
Alisema mamlaka hiyo inafanya kazi ya kutetea na kulinda
maslahi ya wanachama,wafanyakazi na wastaafu ili kuleta faida kwa wateja kwa
kuboresha uhakika wa maisha yao ya baadaye,kinga dhidi ya majanga kwa
watanzania na kukuza uwekezaji nchini.
Naye katibu tawala wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi
alisema utendaji mbovu wa baadhi ya mifuko unakatisha tamaa watumishi kujiunga na mifuko yao, kutokana na
kuona hali halisi jinsi wazee wastaafu wanavyohangaika kufuatilia mafao yao
wakati takwimu zote zipo lakini kwenye malipo inakuwa tatizo.
Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoa wa
Shinyanga (TUCTA)Fue Mlindoko,alisema kero kubwa wanazokumbana nazo ni mafao
kutokuwa sawa miongoni mwa watumishi wakati wakitambua fika tarehe za kuajiriwa
na kustaafu, lakini cha kusikitisha wakati wa kuchukuwa mafao yanakuwa kidogo
kinyume na matarajio yao.
No comments:
Post a Comment