Tuesday, June 24, 2014

WIZI WA JOGOO WAMPONZA BALOZI WA SHINA LA CCM ,ACHINJWA KAMA KUKU NA KUKATWA MIGUU KISHA KUCHOMWA MOTO.





TUKIO:Mjumbe wa shina(Balozi)wa Chama cha mapinduzi(CCM)katika Kijiji cha Ibamba,kata ya Uyovu,Lunzewe Mathayo Kalimanzira(49)ameuawa kinyama na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa kama mbwa mwizi, kukatwa miguu yake yote,kisha kuchomewa ndani ya nyumba yake.

CHANZO: Balozi Kalimanzira amefikwa na kazia hiyo Juni 16 mwaka huu majira ya saa 2 usiku baada ya kutuhumiwa kuiba kuku(jogoo) wa jirani yake ambaye amefahamika kwa jina la SWED SWAHIBU mkazi wa Ibamba, kaya hiyo ya uyovu.

MASHUHUDA: Wameleeza kuwa,Balozi KALIMANZIRA baada ya kuiba kuku huyo alimpeleka nyumbani kwake na kumwamuru mkewe amchinje na kumpika ambapo manyoya yake aliyatupa chooni ili asigundulike.

Kama wahenga wasemavyo,siri ni ya mtu mmoja,pamoja na manyoya kuyatupa msalani,mwenye kuku SWAHIBU,alipata taarifa kuonekana kwa jogoo wake kwa Kalimanzira kabla hajachinjwa.

Wamesema,SWAHIBU alipofika nyumbani kwa KALIMANZIRA,alielezwa kuwa,kuku ameshachinjwa na ndipo alipoingia jikoni kufunua chungu kilichotumika kupikia jogoo wake na kubaini kuwa tayari kuku wake huyo alishabadirika jina na anaitwa supu ya kuku.

Kutokana na hali hiyo,SWAHIBU alipiga yowe kuwaita majirani wajionee hali halisi,na wananchi hawakuwa na suala jingine zaidi ya kujua alipo Balozi huyo ambapo walielezwa kuwa yuko kazini kwake LUNZEWE SENTA ambako anafanya kazi ya ulinzi wa maduka ya wafanyabiashara.

Wananchi hao walimfuata KALIMANZIRA na kumleta nyumbani kwake na baada ya kumhoji alikiri kuiba kuku huyo na akaomba apewe muda ili anunue mwingine kama fidia kwa jirani yake hata hivyo wananchi hao hawakumwelewa na ndipo waliochukua jukumu la kumhukumu kifo.

Kwa mjibu wa mashuhuda wa tukio hilo,wamesema kabla hawajamuua walimpa kipigo kikali hadi alipolainika,kana kwamba hiyo haitoshi walimkata miguu yake yote,kisha wakawaamuru watoto wake kutoka ndani ya nyumba yao.

Imeelezwa mara baada ya watoto kutoka ndani,wananchi hao walimwingiza KALIMANZIRA ndani ya nyumba yake wakamimina petrol kisha wakailipua moto nyumba hiyo na ndipo wananchi hao walipoamua kusambaa eneo hilo kukwepa mkono wa sheria.

MKEWE AZUNGUMZA:RUSI CHIZA mke wa Marehemu KALIMANZIRA,amedai kuwa awali siku hiyo aliona jogoo likiwa na kuku wake wa kike lakini hakujua kama ni wa wizi.

Ameeleza kuwa,mumewe aliporudi jioni kutoka matembezini alishangaa kuona akimchinja jogoo huyo na kumwamuru ampike na kwamba baada ya kumpika alishangaa mwenye jogoo akifuata kuku wake na ndipo alipomueleza ameshachinjwa na manyoya yametupwa chooni.

CHIZA ameongeza kuwa,baada ya kumweleza vile,mwenye jogoo alipiga kelele kuita watu na ndipo walipochukua jukumu la kumfuata kazini kwake na kumrejesha nyumbani kisha kumuua kinyama kwa kukata miguu yake na kumchomea ndani ya nyumba yao mara bada ya watoto wao kutoka nje.

Kwa mjibu wa mke huyo wa marehemu,kwa sasa hawana sehemu ya kuishi kwani mbali na nyumba yao kuteketea kwa moto,pia samani zote za ndani ziligeuka kuwa majibu.

POLISI LAWAMANI: Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Ibamba PASCHAL MICHAEL mbali na kuthibitisha kuwepo kwa tukio hilo amelitupia lawama jeshi la polisi katika kituo cha LUNZEWE kwa kushindwa kufika eneo la tukio kwa wakati mbali na yeye kuwataarifu muda mfupi kabla ya wananchi hawajatekeleza mauaji hayo.

MICHAEL ambaye anadai alikuwa safari,baada ya kupigiwa simu na msamaria mwema aliyemtaarifu uwepo wa tukio hilo alipiga simu polisi lakini cha ajabu polisi wamefika eneo hilo asubuhi wakati tukio limetokea majira ya saa 2 usiku.

 RPC AZUNGUMZA: Kwa upande wake kamanda wa polisi Mkoa wa Geita JOSEPH KONYO yeye amelaani mauaji hayo na kuahidi kumwajibisha mkuu wa kituo cha polisi LUNZEWE kwa kushindwa kufika eneo la tukio mapema kwa kile alichodai iwapo polisi wake wangefika mapema eneo la tukio huwenda mauaji hayo yasingetokea.

Kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu,ambapo wananchi wamekuwa wakiwalalamikia baadhi ya askari wa Kituo hicho kwa kushindwa kufika kwa wakati katika matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani lakini katika matukio ya kukamata wezi wa mafuta ya dizeli na mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu wamekuwa wakifika mapema kisha kupora mali hizo kutoka kwa wahusika.

Story  Na Victor Bariety-malunde1 blog Geita

No comments:

Post a Comment