FISI ALIYESHAMBULIA WATU KWA KUWAUMA MIGUU NA MIDOMO ,WANANCHI WAGOMBANIA NYAMA YAKE BAADA YA KUUAWA NA KUFANYA KUWA KITOWEO.
MATUKIO
yanayohusishwa na imani za kishirikina ya watu kushambuliwa na Fisi
hususani watoto chini ya Umri wa miaka Mitano sasa yamechukua sura mpya
mkoani Geita baada ya fisi mwingine kuvamia mtaa na kuanza kushambulia
watu hovyo kwa kuwauma kabla ya polisi kufika eneo hilo na kumuua kwa
risasi kisha kutoa mwanya kwa wananchi kugombea nyama yake na kuifanya
kitoweo.
Tukio
hilo la kusitaajabisha na ambalo limeacha maswali mengi,limetokea
jana,majira ya saa 9 alasiri katika mtaa wa Kabahelele,Kata ya Katoro
Wilaya ya Geita Mkoani Geita.
Mashuhuda
wa tukio hilo waliuambia mtandao wa malunde1 blog kuwa,mara baada
ya fisi huyo mkubwa mithiri ya Ndama kuvamia kwenye mtaa huo wananchi
walishikwa na taharuki wasijue la kufanya.
Walidai
kuwa,wakiwa wanajiandaa kuchukua hatua dhidi ya Fisi huyo,walishangaa
kuona akivamia watu mmoja baada ya mwingine na kuanza kuwauma na ndipo
walipopiga kelele kisha kukusanyika na kumweka kati mnyama huyo huku
wengine wakipiga simu polisi kuomba msaada.
Wakati
polisi wanafika eneo hilo,tayari Fisi huyo alikuwa amekwishafanya
madhara kwa watu watatu ambao waling’atwa sehemu za miguuni na midomoni
hali iliyowalazimu polisi kutawanya watu kisha walifanikiwa kumuua fisi
huyo kwa kumpiga risasi zaidi ya mbili.
Waliojeruhiwa
na Fisi katika tukio hilo,ni pamoja na Bugamba Zumbe(21),Peter Francis
(32),na mwingine ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja wote
wakazi wa mtaa huo wa Kabahelele.
Hata
hivyo katika hali ya kushangaza baada ya Fisi huyo kuuawa,baadhi ya
wananchi wa eneo hilo nusura wauane kwa kukatana visu wakigombea nyama
ya mnyama huyo na walipohojiwa sababu za kugombea nyama hiyo walidai
inaliwa na kwamba ikipikwa vizuri inazidi hata ile ya ng’ombe.
‘’Ndugu
mwandishi huyu mnyama pamoja na kwamba ni mchafu lakini nyama yake
ikipikwa kwa kuandaliwa vyema ni nzuri kuliko hata ile ya ng’ombe ndiyo
maana unaona watu wanataka kukatana visu lengo kila mmoja apate hata
kipande kimoja maisha yenyewe magumu hapa tumeokoa pesa ya
mboga’’alisema mwanamke aliyefahamika kwa jina moja la Helena mkazi wa
Mtaa huo.
Ofisa
Maliasili wa Wilaya ya Geita Kasika Gamba alidai kuwa,chanzo cha Fisi
kushambulia watu,ni kutokana na uharibifu wa mazingira katika Hifadhi za
Mistu hali ambayo imesababisha wanyama hao kuzagaa kwenye makazi ya
watu kutokana na kukosa sehemu ya kijihifadhi na kujipatia chakula.
Kwa
upande wake Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Geita Thobias
Kiputa,aliwataka wananchi kuepuka kula hovyo nyama za wanyama ambao siyo
wanyama(Meat Animals)ambao ni wala nyama kama Fisi ambao hawajakaguliwa
wanaoweza kuwa na magonjwa mbalimbali yanayoweza kuwasababishia madhara
ya afya na badala yake wajitahidi kula nyama itokanayo na wanyama wa
nyama katika maeneo yao ambao mara nyingi wanakuwa wamekaguliwa na
wataalamu wa mifugo.
‘’Haipendezi
watu kula nyama ya wanyama wala nyama(Meat Animals),kwani wanaweza kuwa
na magonjwa mbalimbali maana fisi ni wanyama wala nyama na wanaweza
kuwa na magonjwa mbalimbali,watu wasipende kula wanyama hao kwa kuwa
wanakuwa hawajakaguliwa na si utamaduni wetu’’
‘’Na
si desturi wataalam kukagua wanyama wa aina hiyo ninachowashauri
wananchi wajitahidi kula nyama itokanayo na wanyama wa nyama kwenye
maeneo yao, ambao mara nyingi wanakuwa wamekaguliwa na wataalamu wa
mifugo’’kwani wanaweza kula nyama ya aina hiyo(Fisi) wakapata madhara
ya kiafya’’alisema Dakta Kiputa.
Mwishoni
mwa wiki iliyopita Mwanaume mmoja mwenye Umri wa miaka 35 mkazi wa
Nyabulanda Tarafa ya Nyang’hwale Wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita
aliuawa kwa kushambuliwa na Fisi na kuliwa,sehemu za Tumbo,mguu mmoja
ukiwa umebaki mfupa na ule wa kulia haupo pamoja sehemu za usoni
kichwani na kifuani.
Matukio ya fisi kushambulia na kula watu yamekuwa yakitokea mara kwa
mara mkoani Geita hasa kwenye Halmashauri za wilaya za Nyang'hwale na
Geita ambapo mara nyingi kundi linaloadhirika zaidi na wanyama hao ni
watoto wenye umri chini miaka 5.
No comments:
Post a Comment