Friday, July 25, 2014
SHEHENA YA MAGUNIA 20 YA BANGI YAKAMATWA IKISAFIRISHWA KWA PUNDA
JESHI la Polisi mkoani Arusha, limekamata shehena ya magunia 20 ya dawa za kulevya aina ya bangi yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 18 ikiwa inasafirishwa kwa punda huku wamiliki wa wanyama hao wakiwa hawajulikani.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, aliwaeleza wandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa walikamata bangi hiyo Julai 23 mwaka huu, majira ya saa 2:30 usiku katika Kijiji cha Olteres, Kata ya Longido wilayani Longido.
Alisema kuwa bangi hiyo ilikuwa ikitokea Oldonyosambu kupelekwa Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya upande wa Arusha, ambako iliwachukua zaidi ya saa sita kufuatilia watuhumiwa hao.
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu wanasafirisha bangi kwa kutumia punda, jeshi hilo kwa kushirikiana na askari wa kampuni ya Jumuiya ya Jamii inayojishughulisha na ulinzi wa wanyamapori na mazingira kambi ya Enduimet, walifanya doria kufuatilia ndipo walifanikiwa kuona punda watano wakiwa na magunia hayo ya bangi.
“Awali waliona nyayo za binadamu pamoja na wanyama aina ya punda zikitokea Oldonyasambu kuelekea Namanga na kuzifuatilia kuanzia saa 8:00 mchana hadi 2:30 usiku na kufanikiwa kuyapata magunia hayo ambayo yalikuwa yametelekezwa na watu ambao bado hawajulikani,” alisema.
Alisema kuwa wanaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wahusika waliokuwa wakisafirisha bangi hiyo sanjari na kuwabaini wengine wenye kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia njia hizo za panya. Via :Tanzania Daima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment