Tuesday, August 26, 2014

SERIKALI YAAMRIWA KULIPA MELI ,SAMAKI WA MAGUFULI

Dk. John Magufuli
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru Serikali ya Tanzania kulipa meli ya uvuvi pamoja na samaki waliokamatwa miaka mitano iliyopita mali ya raia wa China, vyote vikiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 3.2.
Mahakama hiyo imetoa amri hiyo baada ya kuwaachia washtakiwa wawili raia wa China, Hsu Tai na Zhao Hanquing, waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya kuvua samaki katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania bila kibali, maarufu ‘Samaki wa Magufuli’.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Wakili wa Utetezi, Kapteni Ibrahim Bendera, alisema meli iliyokamatwa na wateja wake ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 2.5 na samaki waliokutwa nao walikuwa na thamani ya Dola za Marekani 720,000.

“Bado tunasubiri maelekezo ya wamiliki wa hiyo meli kuhusu hatua za kisheria zinazostahili ili wapate fedha hizo” alisema Kapteni Bendera kwa njia ya simu.

Agosti 22, mwaka huu, Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Isaya Arufani, alisoma uamuzi wa kuwaachia huru Wachina hao, pamoja na mambo mengine, aliamuru serikali kulipa mali hizo pamoja na hati zao za kusafiria.

Kesi hiyo awali ilikuwa ikiwakabili watu 38 kutoka mataifa tofauti ya Bara la Asia ya China, Ufilipino, Vietnam na wawili raia wa Kenya.

Walikamatwa Machi 8, mwaka 2009 wakivua na walikutwa na tani 293 za samaki, wakati huo, Dk, John Magufuli akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Kati ya washtakiwa hao, mmoja alifariki dunia, wengine 35 waliachiwa huru na wawili kutiwa hatiani.

Hakimu Arufani aliwaachia huru washtakiwa hao wiki iliyopita ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka hayo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment