Friday, August 8, 2014

WAGOMA KUHIFADHI MAZAO GHALANI BAADA YA KUUZA KWA BEI YA HASARA.




 WAKULIMA wa zao la mpunga katika kijiji cha Nyida halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,wamekataa kuendelea  kuhifadhi zao hilo katika ghala lililopo kijijini humo
kutokana na kuuza kwa bei ya hasara  mwaka jana  huku  waliouza   kikohela bila kuhifadhi  maghalani wakipata  faida.

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya  wakulima wa kijiji hicho walisema hali hiyo imewakatisha  tamaa kwani walitarajia hali itakuwa nzuri kwa kuwa na soko lenye tija kwao,ambapo waliuza gunia sh 45,000 ikilinganishwa na ambao hawakuweka kwenye maghala waliuza kwa sh 75,000 hivyo kupata faida.

  Mariamu Manosha ni mkulima wa mpunga kutoka kijiji cha Nyida alisema wanajitahidi kulima kwa bidii zao hilo,lakini  changamoto zilizopo zinawakatisha tamaa ikiwa ni pamoja na kukosekana  maji ya uhakika kwani wanategemea mvua za masika ambazo wakati mwingine zinakuwa za wastani ikiwa ni pamoja na na kuuza kwa bei ya hasara.

Naye  mkulima  ambaye pia  ni mjumbe wa bodi  ya zao la mpunga taifa (RCT )  Luhende  Malija alisema kuwa,  bado kunachangamoto kubwa kwa wakulima  kwani hawajaingia kwenye mfumo wa kilimo cha  kisasa sababu kunachangiwa na shida ya maji katika uzalishaji ikiwemo mbegu za kisasa kuuzwa kwa bei kubwa.

Luhende alisema kuwa  mwaka jana  wakulima walijitokeza kuhifadhi kwa kuhamasishwa na shirika lisilo la kiserikali la Rudi kuweka mazao ghalani na kupima kwenye  mizani ,ambapo wakulima waliweka  gunia 232 kwa msimu huo  huku changamoto ikijitokeza wakati wa  uuzaji kwani walisubiri  soko kuwa zuri  matokeo yake waliuza shilingi 45,000 kwa gunia moja

Kwa upande wake afisa mtendaji wa  kata ya Nyida  Kadushi Deogratius  alisema  awali wakulima waliona  bei ya shilingi 75,000 ni nzuri  na kuanza kutunza ghalani  wakiwa na imani  huenda itapanda zaidi ya hapo matokeo yake ilishuka na kufikia shilingi 45,000 kwa gunia moja mpaka sasa hakuna zao lolote kwenye ghala.

 Afisa kilimo na mifugo wa  kata hiyo Selemani  Msunga alisema kuwa kata hiyo inavijiji vitatu  ambavyo ni  Nyida,Nduguti na Igembya  ambapo idadi ya kaya ziizopo ni  1440  zinazojishughulisha na kilimo cha zao hilo  huku eneo linalofaa kwa kilimo   cha mpunga  hekta 700  na kwamba uzalishaji  umeshuka kutoka  magunia 30 hadi magunia 12 kwa hekta moja.

Alisema  kunatokana na upungufu wa mazao  wanayovuna wakulima  na  kukosa uhakika wa soko imara ,kwani wakulima wao walitegemea  kuhifadhi ghalani kutapatikana  soko la uhakika,lakini  matokeo yake  hali imekuwa tofauti hivyo kuona  hakuna faida  na hakuna zao lolote lilowekwa ghalani kama ilivyokusudiwa kuwepo kwa ghala hilo.
                         Na Stella Ibengwe

No comments:

Post a Comment