Friday, August 22, 2014

WANAOCHOCHEA MAUAJI YA ALBINO WAONYWA

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),Isaya Mngulu.
Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kwa wale wanaoshawishi uhalifu na  kukemea matukio ya kihalifu yaliyoibuka hivi karibuni kwa kuwajeruhi watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, alisema  ili kudhibiti matukio hayo kunahitajika ushirikiano kutoka kwa jamii na wadau wengine kwa kutoa taarifa.

Alisema kuwa katika kipindi cha miezi minane mwaka huu kumetokea matukio matatu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

 “Jeshi la Polisi  linaendelea na operesheni ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wale waliopo kwenye   mtandao wa mauaji hayo, wakiwamo waganga wa jadi hususani wapiga ramli,”alisema Mngulu.

Aidha, alisema  Jeshi hilo  linaiomba jamii kutoa taarifa za wahalifu katika kituo chochote cha polisi pamoja na kupiga simu namba 0754 78 55 57.

Alisema Mei 12, mwaka huu  aliuawa Munhgu Lugata, mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu na Jeshi la Polisi tayari limefanikiwa kuwakamata watu saba kuhusiana na tukio hilo.

Agosti 5 na 16, mwaka huu, Pendo Senerema na Mungu Massaga, wakazi wa mkoani Tabora walikatwa mikono kwa nyakati tofauti  na watu wasiojulikana.

   Chanzo: Nipashe
 

No comments:

Post a Comment