Sunday, September 14, 2014

AUAWA KIKATILI KWA KUCHOMWA KISU TUMBONI NA KUTOLEWA UTUMBO NJE BAADA YA KUTOA MSAADA

Mkazi wa Kijiji cha Ilogi, wilayani Kahama, Ester Bundala (80), ameuawa kikatili kwa kuchomwa kisu tumboni na kutolewa utumbo baada ya watu waliojifanya wagonjwa kwenda nyumbani kwake kuomba msaada wa kuchemshiwa dawa.

Wauaji hao pia walimchoma bibi huyo kisu sehemu ya moyo, mbavu na mkono wa kulia na kutokomea kusikojulikana.

Mtoto wa bibi huyo, Francis Paulo, alisema wauaji hao ambao walikuwa wawili, walifika nyumbani kwao Ijumaa iliyopita saa 12 jioni wakilalamikia kuumwa tumbo na kuomba msaada wa kuchemshiwa maji ili wachanganye na dawa waliyokuwa nayo kujitibu.

Paulo alisema mama yake aliwachemshia maji na kuwapa ili waweze kutengeneza dawa yao na baada ya kunywa walipumzika wakisubiri wapate nafuu.

“Baadaye giza lilipoingia baba yangu mzee Paulo Nshimbi (83) alikuja nyumbani kwangu kukamua maziwa kwa vile sikuwepo na ndama walihitaji kupewa maziwa,” alisema Paulo.

Anasimulia kuwa kitendo cha mzee wake kuwaaga wageni kilitoa mwanya wa kumuua mama yake.

“Hata hivyo muda mfupi kabla hajakata roho mzee alirejea na kumkuta mama anahangaika, utumbo ukiwa umetoka nje, amepoteza damu nyingi na kumtajia jina...."fulani amenichoma kisu amekuja kuniua”, alinukuu maneno aliyosema mama yake huku akitaja jina la muuaji (jina linahifadhiwa).

Aliongeza kuwa muuaji alitumia mbinu ya kukodi wageni hao alioshirikiana nao kumuangamiza mama yake kwa vile alifahamu ratiba ya siku hiyo.

Paulo alisema siku ya mauaji yeye na shemeji yake anayeishi na wazazi wake, alikwenda kijiji cha jirani cha Bugarama kumsalimia mkwe wao aliyekuwa mgonjwa.

Alisema walitoa taarifa kituo cha polisi Bugarama na watuhumiwa wandugu Andrea na Robert Mabala wamekamatwa lakini mhusika ambaye ni mwanafamilia aliyetajwa na mama yao wakati anakata roho hajaonekana.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanya, Musa Athumani Taibu, alithibitisha kuwapo kwa mauaji hayo na kueleza kuwa mtuhumiwa ametoroka na polisi inaendelea na msako.
NA GAUDENSIA MNGUMI-nipashe jumapili

No comments:

Post a Comment