Monday, September 15, 2014

SHULE YA SEKONDARI YA KATA MWENDAKULIMA YAFANYA MAAJABU


Wanafunzi wa shule ya sekondari Mwendakulima wilayani Kahama mkoani Shinyanga(waliohitimu na ambao bado wako shuleni)



Jamii imetakiwa kuacha mara moja tabia ya kudharau na kubeza shule za sekondari za kata kwa madai kuwa hazifanyi vizuri katika matokeo ya mitihani kwani zipo shule zilizoonesha mfano mzuri ikiwemo shule ya sekondari Mwendakulima iliyopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambayo imefaulisha wanafunzi wake wote wa kidato cha sita mwaka 2014 kwa kupata daraja la kwanza na pili pekee.

Rai hiyo imetolewa juzi na meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi uliopo Kahama unaomilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya African Barrick Gold bwana Philbert Rweyemamu wakati wa hafla maalum iliyoandaliwa na mgodi huo kuwapongeza wanafunzi 15 waliokuwa wanawafadhili kupitia mradi wake uitwao “Can Educate katika shule ya Sekondari Mwendakulima.

Rweyemamu alisema shule ya sekondari Mwendakulima inastahili kupongezwa kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa na kanda ya magharibi na nafasi ya 9 kitaifa kati ya shule 180 zenye wanafunzi wachache katika matokeo ya kidato cha 6 kwa shule zenye wanafunzi wachache.

“Tumekuja hapa kwa sababu ya matokeo mazuri ya vijana hawa,shule imefanya maajabu,wanafunzi wote wamefaulu vizuri,pamoja na mchango wa mgodi pia walimu wamejitahidi,huu ni mfano wa kuigwa acheni kubeza shule za kata”,aliongeza Rweyemamu.

“Hawa ni mashujaa wetu,wengi wanatoka kwenye familia maskini,wanaosema shule za kata hazifai sijui wataficha wapi aibu yao,naomba wadau wote tuzisaidie shule hizi,hili suala siyo la mgodi pekee,huu ni muda wa kuwa na mapinduzi katika sekta ya elimu”,alieleza meneja huyo wa mgodi wa Buzwagi.

Naye mkuu wa shule hiyo bi Dianal Kuboja alisema jumla ya wanafunzi wa kidato waliomaliza masomo yao mwaka huu walikuwa 23,kati yao 15 walikuwa wanasomeshwa na mgodi na wote wamepata daraja la kwanza huku 8 waliobaki wakipata daraja la pili.

Hata hivyo mbali na kuushukuru mgodi kwa kusaidia ada,sare na vifaa vingine muhimu vya shule kwa wanafunzi kutoka familia zenye kipato duni aliomba wadau mbalimbali wa elimu kuona umuhimu wa kuwasaidia chakula na malazi wanafunzi ili kuendelea kuwa matokeo mazuri.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha sheria kutoka African Barrick Gold bi Catrine White ambaye pia nimkurugenzi wa bodi ya ufadhili katika mradi wa Can Educate alisema wataendelea kutoa msaada kwa wanafunzi wasiojiweza na kwamba mwaka huu jumla ya dola 100,000 zimetengwa kusaidia wanafunzi wenye mahitaji.

“Mradi umeanza mwaka 2013 mwaka huu,tumefarijika na matokeo mazuri ya vijana hawa,pesa zetu zinatumika vizuri,nawaomba waliobaki wajitume zaidi,hapa Kahama tunasomesha wanafunzi zaidi ya 400”,alieleza White.

Naye afisa elimu taaluma sekondari halmashauri ya mji Kahama Richard Msagati aliyemwakilisha mkurugenzi wa halmashauri hiyo aliwataka wanafunzi wanaonufaika na mradi huo wasome kwa bidii na kuongeza kuwa matokeo mazuri yanaifanya pia shule kuheshimika katika jamii.

Nao wanafunzi waliomaliza kidato cha sita katika shule hiyo mbali na kuupongeza mgodi wa Buzwagi kwa kujali sekta ya elimu nchini pia waliiomba kuwafikia wanafunzi wengi zaidi ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata haki ya elimu.

Jumla ya wanafunzi 15 wa kike waliopata daraja la kwanza waliokuwa wanasomeshwa na mgodi walipewa vyeti huku walimu wakipewa vikombe vya ajabu vinavyobadilika rangi ukiweka maji ya moto wakati wa hafla hiyo maalum iliyofanyika katika shule ya sekondari Mwendakulima iliyopo katika kata ya Mwendakulima katika halmashauri ya mji Kahama

No comments:

Post a Comment