Kiwango kikubwa cha Sukari kinagharimu sekta ya afya na kuwaathiri zaidi watoto..
 
Wataalamu wa afya wanatahadharisha kuwa juhudi zaidi zinahitajika kupunguza kiwango cha Sukari kinachotumiwa na watu.

Shirika la afya duniani kwa ushirikiano na washauri wa maswala ya afya nchini Uingereza, wamependekeza kupunguza viwango vinavyopendekezwa vya kutumia sukari mwilini.

Ushauri mpya unasema kuwa kiwango kinachostahili cha Sukari mwilini ni asilimia 5 kutoka asilimia 10.

Lakini utafiti mbadala unasema kwamba kiwango kinachofaa hakipaswi kuwa zaidi ya asilimia 3.
Watafiti wanasema kuwa ushauri huu mpya unahitajika ikizingatiwa gharama ya matibabu kwa sekta ya afya hasa matibabu ya magonjwa ya Meno.

Wanasema kuwa Sukari ni kiungo muhimu zaidi katika kuchochea magonjwa ya Meno kwa sababu ya hilo, ni ugonjwa ambao unaweza kuzuilika.

Utafiti unaonyesha kuwa kutumia kiwango kikubwa cha Sukari mwilini kunaongeza uwezekano wa meno kuoza na kuharibika hususan kwa watoto.

Matibabu ya magonjwa ya Meno hugharibu nchi zilizostawi kati ya asilimia 5 na kumi ya matumizi ya pesa za matibabu.
Wataalamu wanasema kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa kwa haraka.

'Kodi kwa Sukari'
Wataalamu wanataka serikali kudhibiti upatikanaji wa mashine za kuuza soda na vinywaji vingine vyenye sukari na hata kuyaondoa katika maeneo ya shule na hospitali.

Pia wanasema kuwa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha sukari vinapaswa kuwekwa vibandiko na serikali kuvitoza ushuru mkubwa.
Wanasema kuwa swala la watu kutumia sana Sukari ni tatizo kubwa kwa umma.

Licha ya hatua kuchukuliwa kupunguza matumizi ya Sukari, takwimu zinaonyesha kuwa watu wengi bado wanatumia kiwango kikubwa cha Sukari.
 Via :BBC