Ndugu wa mtu anayedaiwa kuwa ni mlemavu wa akili, Galus Focus Nguruwe
(35) ambaye ni mwalimu wa sekondari moja mjini Morogoro, wamelituhumu
Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship lililopo
Boko Magengeni jijini Dar kuwa wamemfunga mnyororo ndugu yao huyo kwa
miezi nane mfululizo.
Mwalimu Galus Focus Nguruwe akiwa amefungwa mnyororo
Kwa mujibu wa dada wa Galus, Piencia Focus, ndugu yao huyo alichukuliwa
na mke wa mtoto wa dada yao waliyemtaja kwa jina la Doreen kutoka Songea
mkoani Ruvuma Januari, mwaka huu bila kuwataarifu ndugu, jambo
lililowafanya wamfuatilie na kugundua alipelekwa kwenye kanisa hilo kwa
madai ya kufanyiwa maombi.
Dada wa Galus, Piencia Focus akiwa kanisani hapo
Dada huyo alisema kuwa
aliamua kumtafuta ndugu yake hasa baada ya kupata taarifa kuwa aliko
amekuwa akishinda huku amefungwa mnyororo mguuni, hali inayomfanya
ajisaidie na kula papohapo.
“Japokuwa alikuwa na
matatizo ya akili tangu zamani, lakini alikuwa akitumia dawa zake na
alipata nafuu na kufanya kazi yake ya ualimu kwani alikuwa akifundisha
shule moja ya sekondari Morogoro,” alisema Piencia Focus.
Kaka wa Galus,Peter Focus akizungumza na waandishi wa habari.
Naye kaka wa Galus, aliyejitambulisha kwa jina la Peter alisema baada ya
kupata taarifa kwamba mdogo wake yupo kwenye kanisa hilo aliamua kufika
kwa ajili ya kumchukuwa kistaarabu lakini cha kushangaza alijikuta
akiangukia kwenye mikono ya waumini hao wakidai yeye ni gaidi na
wakamkwapulia fedha zake.
Peter alisema alipoachiwa alikimbilia Kituo cha Polisi Wazo Hill ambapo alifungua jalada lenye Namba za Kumbukumbu WH/RB/6364/14 WIZI TOKA MAUNGONI.
Waumini wa kanisa hilo wakijibizana na ndugu wa Galus kanisani hapo.
Peter alisema alilazimika kuungana na dada yake kwa kushirikisha na
vyombo vya usalama ambapo walifika kanisani hapo kwa mara nyingine ili
kumkomboa ndugu yao na kuwatia mikononi waumini waliomwibia fedha zake.
Waandishi wetu waliokuwa karibu na eneo hilo walizinyaka taarifa hizo na
kufika kanisani hapo ambapo waliwashuhudia ndugu hao wakiwa na polisi
wakimchukuwa mmoja wa watuhumiwa waliodaiwa kumshambulia Peter na
kuondoka naye.
Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship kwa muonekano wa mbele.
Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kitendo cha polisi hao kumwacha Galus
akiwa bado amefungwa kwenye nguzo na mnyororo kanisani hapo wakidai
watamfuata baada ya kumpeleka mtuhumiwa wa unyang’anyi kituoni, jambo
ambalo halikuwa la kweli kwani hawakufika kwa siku hiyo.
Waandishi wetu walishuhudia timbwili la aina yake kanisani hapo kati ya
waumini wa kanisa hilo na ndugu wa Galus waliorejea kwa lengo la
kumchukuwa ndugu yao baada ya awali kumpeleka kituoni mtuhumiwa wa
kumshambulia Peter.
Waandishi wetu walipoomba kuzungumza na uongozi wa kanisa hilo
ilishindikana na kujikuta wakishambuliwa kwa maneno huku wakitakiwa
kuondoka mara moja katika eneo la kanisa hilo.
Waandishi: Hamida Hassan, Gladness Mallya, Chande Abdallah na Deogratius Mongela.
No comments:
Post a Comment