Friday, October 31, 2014

ADAI FIDIA YA MBUZI 30 TU ILI AMSAMEHE MWANAUME ALIYEMFUMANIA NA MKE WAKE


MWANAMUME wa makamo anadai fidia ya mbuzi 30 kutoka kwa mwanamume aliyefumaniwa nyumbani kwake akifanya mapenzi na mkewe.
Bw Harun Waithaka, mwenye umri wa miaka 28, ambaye ni baba wa watoto wawili alimfumania mwanamume huyo usiku wa kuamkia Alhamisi na baada ya kukatazwa kumuua, akasema basi alipwe fidia hiyo.
Hata hivyo, kulizuka kizaazaa pale mkewe alipomtetea wanamume huyo akidai kuwa alikuwa akisononeka kimapenzi kwa kuachwa kwa muda mrefu pekee yake.
Kisa hiki kilitokea katika kijiji cha Kaganda, Kaunti ya Murang’a.
“Bw Waithaka ambaye hufanya vibarua katika mji wa Garissa alikuwa akipata habari kuwa mwanamume huyo alikuwa mpenzi wa mkewe Bi Florence Wanjiru (umri wa miaka 24) na ndipo akaamua kuthibitisha,” akasema Bw Joseph Gathuri ambaye ni mwenyekiti wa mpango wa kiusalama wa Nyumba kumi.
Bw Waithaka katika harakati ya kuthibitisha fununu hizo, aliwaomba watu kadhaa wakae macho wakichunguza kinachoendelea nyumbani kwake na siku ile ambapo tu wangepata mwanamume huyo kwake, wamjulishe mara moja.
“Nilikosa kurudi kazini Garissa na badala yake nikakodisha chumba cha malazi katika mji wa Murang’a nikingoja kupashwa habari kuwa mwanamume huyo ameonekana akiingia kwangu,” akasema Bw Waithaka.
Ndipo Jumatano usiku mwendo wa saa tano alipokea simu kutoka kwa jirani yake akimwarifu kuwa mshukiwa alikuwa tayari ameingia ndani ya nyumba hiyo.
Alisema alikodisha teksi ambayo ilimpeleka hadi karibu na boma lake huku akiwa na upanga.
Aliongeza pia kuwa aliwaita majirani kadhaa ambao pia walijumuisha mwanasiasa wa eneo hilo Bw David Ng’ang’a na kuvunja mlango wa nyumba hiyo.
Asichukue sheria mikononi
Hata hivyo, viongozi wa Nyumba Kumi walimhimiza asichukue sheria mikononi mwake bali afuatilie haki katika kanuni na utaratibu wa sheria.
“Ndipo ikawa mwanamume huyo apigwe faini kulingana na mila na desturi za jamii ya Agikuyu,” akasema Bw Gathuri.
Waliandikiana mkataba ambao unamhitaji mume huyo alipe mbuzi hao kwa awamu tatu katika kipindi cha miezi sita ijayo ambapo gharama hiyo ilikadiriwa kuwa ya Sh45, 000.
Kamishna wa kaunti hiyo Bi Kula Hache alisema maafisa wake walipashwa habari kuhusu tukio hilo lakini wakaambiwa suluhu ilikuwa imepatikana.
“Tuliagiza washirikishi wa kiusalama katika kijiji hicho wasikubalie sheria ichukuliwe mikononi ila wakatwambia suluhu ilikuwa imepatikana,” akasema.
Bi Hache alisema eneo hilo huwa na visa vingi kama hivyo na ambavyo huwa vinatatuliwa na wazee wa vijiji kwa mujibu wa mila.
 Via: Eddyblog

No comments:

Post a Comment