WALIMU 422 WAFUTWA KAZI, WAMO WALIOFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI WAO
Jumla ya walimu 422 wamefutwa kazi kwa makosa mbalimbali ikiwemo
kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi kwa kipindi cha mwaka
2013/2014.
kiwango cha walimu wanaokwenda kinyume na maadili na kufutwa kazi
kimeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo katika kipindi cha mwaka
2013/2014 walimu 422 wamefutwa katika maeneo mbalimbali nchini,
wakiwemo watatu kwa kubainika kujihusisha kimapenzi na wanafunzi na
wawili kwa kuwaonesha wanafunzi mitihan, ikilinganishwa na walimu 278
mwaka 2012/2013.
Katibu msaidizi wa idara ya utumishi wa walimu, Christina Hape,
amesema hayo mjini Morogoro, na kubainisha kuwa mwaka 2012/2013
walifutwa kazi asilimia 98 ya walimu 151 ambao mashauri yao yalipelekwa
katika idara hiyo kwa mapendekezo ya kufutwa kazi, ambapo amesema sababu
kubwa ya walimu kufutwa kazi ni utoro unaotokana na wengi kwenda
kujiendeleza kielimu bila ruhusa ya mwajiri.
Amesema makosa makubwa yakiwemo ya mwalimu kubainika kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi ama kuonesha mitihani, husababisha
mwalimu kufukuzwa kazi sambamba na utumishi serikalini na binafsi, huku
makosa mengine kama utoro, mwalimu akifukuzwa kazi na kuachiwa utumishi
wake.
Naye kaimu katibu mkuu wa tume ya utumishi wa umma, ambaye pia ni
naibu katibu idara ya utumishi, Rose Elipenda, ametoa wito kwa waajiri
kusimamia vyema utumishi wa watumishi, kwa kuzingatia sheria, taratibu
na kanuni za kazi na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika
maeneo yao ya kazi kabla ya kufikisha mashauri yao katika mamlaka za juu
kwa maamuzi zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya utumishi wa walimu, watumishi hao
wanapaswa kuhakikisha wanatii mamlaka za kisheria zilizowaweka katika
nafasi zao sambamba na kuzingatia kuwa ualimu sio taaluma pekee bali
pia suala zima la maadili kwani wakimpotosha mtoto wanayeaminiwa
kumjenga kiakili, ni kupotosha taifa zima.
No comments:
Post a Comment