MSONGO wa mawazo umesababisha mwalimu wa shule ya msingi Mwang’osha iliyopo kata ya nyamalongo wilaya ya shinyang mkoani hapa Christipian Mafuru (24),kufariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani katika choo cha nyumbani kwake.
Akizungumzia tukio hilo mwalimu mkuu wa shule hiyo Frida Maleko alisema mwili wa mwalimu huyo ulikutwa juzi majira ya saa tisa na nusu alasiri akiwa amejinyonga baada ya kukaa muda mrefu bila kumuona shuleni.
Mwalimu mkuu alisema baada ya kukaa muda bila kumuona ndipo alichukua jukumu la kumpigia simu ambayo iliita bila ya kupokelewa na kuamua kuondoka na walimu wenzake kwenda nyumbani kwake ambapo walikuta mlango umefungwa.
Kufuatia hali hiyo iliwatia mashaka na kuamuwa kuvunja dirisha la nyumba hiyo ambapo hawakukuta mtu ujumbe wa maneno ulioandikwa kwenye Barua na kuwekwa mezani uliokuwa umeandikwa na marehemu.
Ujumbe huo ulikuwa ukisomeka kuwa ‘’Msongo wa mawazo umenilazimu nifanye hivi, poleni sana walimu wenzangu,samahani wazazi wangu,kwa heri mwanagu Ray” hali ambayo iliwatia hofu kubwa.
Mwalimu mkuu alisema Marehemu aliajiriwa mwaka jana kwenye shule hiyo na alikuwa mchapakazi aliomba zamu zote za walimu azifanye yeye ili apate uzoefu wa kazi, lakini walishituka baada ya kutomuona muda mrefu shuleni .
“Tulipomkosa nyumbani kwake na kuona ujumbe ambao ulitutisha tulishauriana na walimu wenzangu tukaona ni vema tumtafute hivyo kuchukua jukumu la kuanza kumtafuta na ndipo tuliukuta mwili wake ndani ya choo kajinyonga na ikabidi kutoa taarifa polisi”alisema Mwalimu Maleko.
kamanda wa jeshi la polisi mkoani shinyanga kamishina mwandamizi wa jeshi la polisi (SACP) Evarist Mangala, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema chanzo cha kifo hicho ni msongo wa mawazo wa mwalimu huyo kutokana na barua aliyoandika yeye mwenyewe kwa mkono wake na kutia saini .
Katika tukio hilo hakuna mtu aliyeshikiliwa na jeshi la polisi kuhusiana na kifo hicho,ambapo mwili wa marehemu umeagwa jana shuleni hapo na kusafirishwa kwenda nyumbani kwao wilayani sengerema mkoani mwanza kwa mazishi.
No comments:
Post a Comment