Shinyanga.
ASILIMIA kubwa ya
wajasiliamali hapa nchini hawajajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, hali
inayofanya kukosa fedha za kuwasaidia katika maisha yao hasa
pale wanapopatwa na matatizo kutokana na kuwa na kipato kidogo.
Hayo yalielezwa jana na mjumbe wa bodi ya mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PSPF )kutoka
jijini Dar es salaam Clement Mswanyama,
alipokuwa akitoa elimu kwa wajasiliamali
wa soko kuu la mjini Shinyanga juu ya
umuhimu wa kujiunga na mifuko hiyo na kuwataka
kuchukuwa hatua ili kufanya
mabadiliko katika familia zao sanjari na kujiwekea akiba ya uzeeni.
Mswanyama alibainisha kuwa
watu wanaofanya shughuli zenye kipato kidogo wamekuwa wakisahaulika kupewa fursa ya
kujiunga na mifuko hiyo ,kwa kuwathamini watumishi ambao wameajiriwa hivyo huwajengea watu hao mazingira ya kuwa na
maisha magumu.
“Mfuko wa hifadhi ya jamii utakusaidia kujiwekea hazina ya fedha ambazo zitaboresha
maisha yako hasa pale anapopatwa na
matatizo ya kifamilia ,pia manufaa mengine ya kujiunga ni kupata mafao ya uzeeni na
kuendelea kuwa na maisha mazuri” alisema Mswanyama.
Alisema hapo awali shirika hilo la PSPF lilikuwa
linahudumia watumishi wa serikali pekee,
lakini kutokana na kuona idadi kubwa ya wafanyabishara wa kujitegemea
kusahaulika katika mpango huo na
kunyimwa fursa, ndipo waliamua kupanua
wigo na kuwapa nafasi wajasiliamali kuchangia fedha kidogo shilingi Elfu kumi
kwa kila mwezi .
Kwa upande wake
meneja wa Shirika hilo mkoani Shinyanga Erick Chanimbaga, alisema
wameamua kutoa elimu kwa wajasiliamali wote wa mkoa huo kwa kushirikisha wafanyabishara wa masoko,
mama Lishe,waendesha bodaboda, wafanyakazi wa viwandani ili kuwajengea msingi
mzuri wa maisha kutokana na utunzaji wa fedha katika mifuko ya hifadhi ya
jamii.
Nao baadhi ya wajasiliamali wa soko hilo
Rehema Pius na Daniphod Mshumbusi,walisema elimu waliyoipata
itawasaidia kufanya maamuzi mazuri ya kuchagua mifuko ya hifadhi ya jamii ya
kujiunga nayo ili kujiwekea akiba ya uzeeni pia kusaidia familia wakati wa
shida kwa kuwa kipato chao ni kidogo.
“Leo nimepata uelewa zaidi juu ya mifuko hii ya jamii siku
zote nilikuwa najiuliza maswali mengi lakini sipati majibu,sasa kupitia elimu
hii iliyotolewa na PSPF nimeelewa ,licha ya vipato vyetu ni vidogo sisi
wajasiliamali kumbe tunaweza tu kujiunga
na kulipia kiasi kidogo kila mwezi”alisema Rehema.
No comments:
Post a Comment