Marehemu Mathias enzi za uhai wake.
|
Marehemu Mathias aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na kaka yake wa kuzaliwa,Johnson Damian Mkude.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia
mfanyabiashara maarufu wa Wilaya ya Mvomero, Johnson Damian Mkude (39)
akituhumiwa kumkata kichwa mdogo wake wa kuzaliwa, Mathias kisha
kuondoka nacho kwenda kwa mganga kwa kile kilichodaiwa ni kufanyiwa dawa
ili awe bilionea, mkasa wote huu hapa.
Tukio hilo ambalo kwa sasa ndiyo gumzo mkoani humo lilijiri usiku wa Agosti 3, mwaka huu katika
mashamba ya Kata ya Mlali ambapo ndugu wa marehemu waliokuwa wakimsaka
ndugu yao walifanikiwa kuona kiwiliwili Agosti 6, mwaka huu.
MWILI WAZIKWA KATIKA SHAMBA LA MTU
Mwandishi wetu alifika eneo la tukio na kushuhudia kiwiliwili kikiwa kimeharibika vibaya.
Ilibidi
baba wa marehemu, mzee Damian Mathias Mkude (63) amwombe mmiliki wa
shamba hilo lililopo kwenye Kijiji cha Mbalala, Kata ya Mlali kumzika
mwanaye hapo ambapo alikubali.
BABA WA MAREHEMU
Akizungumzia tukio hilo kwa uchungu, baba wa marehemu mzee Mkude alisema:”Mwezi mmoja kabla ya tukio,
Johnson alinichonganisha na Mathias, nakiri hadi marehemu anakufa
nilikuwa sina uhusiano naye mzuri kutokana na maneno aliyoniambia kaka
yake
“Lakini
nilipomuuliza kuhusu hayo maneno, Mathias alikanusha, nikaamua
kuyafanyia uchunguzi. Wakati naendelea na uchunguzi Agosti 3, mwaka huu,
majira ya jioni, giza halijaingia niliwaona wanangu (Jonson na Mathias)
wamepakizana kwenye bodaboda.
“Siku
hiyohiyo, saa 5 usiku, mke wa Mathias, Revina Evarist akaja kwangu na
kunijulisha kwamba mumewe hajarudi nyumbani na si kawaida
yake kufika muda huo. Tulipompigia simu hakuwa hewani. Kwa vile
nilimuona akiwa na kaka yake, nikampigia yeye lakini simu yake ilizimwa.
“Ilipofika
saa 7 usiku tukaamua kwenda kwa kaka yake, tukamkuta. Nilipomuuliza
mdogo wako yuko wapi akasema hajui. Akajiunga na sisi, tukaendelea
kumtafuta mdogo wake kwa zaidi ya siku 2 bila mafanikio,” alisema mzee
huyo.
MAITI ILIVYOONEKANA
Mzee huyo akasema Agosti 6, mwaka huu alipata taarifa kwamba kuna maiti imeonekana kwenye mashamba ya Mlali.
“Nilishtuka sana kusikia hivyo, nikamtuma
mkwe wangu, mume wa mtoto wangu mkubwa na mtoto wa dada yangu, Gasper
Msimbe. Walisafari hadi Kata ya Mlali kushuhudia maiti hiyo.
“Walipofika waliikuta maiti haina kichwa lakini walimtambua kuwa ni Mathias
kwa nguo na viatu. Walinijulisha haraka ambapo nilikwenda eneo la
tukio. Nilipofika niliumia sana kushuhudia mwanangu asiyekuwa na hatia
kauawa kikatili huku mwili wake uliokuwa hauna kichwa ukitoa harufu kali
kwa kuharibika.”
BAADA YA MAZISHI
“Sasa
kilichonishangaza ni kwamba, baada ya mazishi kule shambani, zimesikika
tetesi kuwa, Johnson ndiye aliyemchinja mdogo wake na kutoweka na
kichwa kwa imani za kishirikina ili awe tajiri mkubwa.
“Nikaambiwa anashikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Mzumbe (kabla ya kupelekwa mkoa). Nilikwenda, nikamkuta amewekwa chini ya ulinzi huku akiwa na hirizi alizokamatwa nazo akiwa kwa mganga wa kienyeji eneo la Sangasanga, Mvomero.”
BABA AOMBA KICHWA CHA MWANAYE
“Pale kituoni, polisi walinitaka nimsalimie lakini nikakataa mpaka arudishe kichwa cha mdogo wake. Tena naliomba
jeshi la polisi kumbana Johnson ili kama kweli amechukua kichwa cha
mdogo wake akirudishe nikizike hapa nyumbani Kijiji cha Nyandila,”
alisema mzee huyo.
MKE WA MTUHUMIWA AZUNGUMZIA KUFUNGA NDOA
Mwandhi
alifika nyumbani kwa Johnson ambapo mke wa mtuhumiwa, Mchilo Peter (33)
alikiri mumewe kuswekwa mahabusu akituhumiwa kumkata kichwa mdogo wake.
Alipotakiwa kueleza chochote kuhusu tukio hilo, mwanamke huyo alisema kwa mafumbo:
“Huko
ni kukosa elimu, kwa nini mganga akudanganye. Kama ni gari mbona yeye
hana, mume nimeanza kuishi naye tangu mwaka 2000, namwambia tufunge ndoa hataki, Jumapili kusali hataki, yuko bize kusaka pesa.
“Siku ya tukio kachukua pesa zote ndani zaidi ya shilingi laki 7. Leo baada ya njaa kuwa kali nimeamua
kufungua duka licha ya kupokea vitisho kwamba kuna kundi la watu
linataka kuvamia duka kwa lengo la kuchoma moto kama hawatapewa kichwa
cha Mathias,” alisema mama huyo.
Alipoulizwa kuhusu mali wanazomiliki, alisema wana nyumba, duka na nguruwe wawili.
MTUHUMIWA ALIJULIKANAJE?
Kwa
mujibu wa Diwani wa Kata ya Nyandila (Chadema), Peter Joseph Zengwe,
Agosti 15, mwaka huu baada ya mauaji hayo kutokea, vijana wawili, Amos
na Mohamed Chali walikamatwa na polisi wakidaiwa kuhusika na mauaji
hayo.
“Siku chache baada ya mauaji hayo, Amos na Mohamed Chali walifuja pesa kwa kunywa pombe kupita kiasi ambapo mmoja aliropoka kilabuni kwamba walilipwa fedha nyingi kwa kumuua Mathias.
“Baada
ya majigambo hayo, watu wakatoa taarifa polisi na wahusika wakakamatwa
na ndiyo waliomtaja Johnson,” alisema diwani huyo.
MGANGA AINGIA MITINI
Mwandishi
alifanikiwa kufika Sangasanga kwa mganga huyo na kuambiwa kuwa
alikimbia kwa kutumia mlango wa nyuma baada ya polisi kufika kwa ajili
ya kumkamata.
MATUMIZI YA KICHWA
Habari
zilizoenea kwenye kijiji alichokuwa akiishi marehemu Mathias zinadai
kwamba, mganga huyo ambaye jina halikujulikana mara moja, alimwambia
mtuhumiwa kuwa, angekifanyia dawa kichwa hicho ambapo angekiweka dukani
ili kuvuta wateja wengi kwa siku, hivyo ndani ya mwaka mmoja tu angekuwa
bilionea.
GPL.
No comments:
Post a Comment