Saturday, August 2, 2014

APOTEZA FAHAMU BAADA YA KUPEWA KARANGA AKIWA NDANI YA BASI


Mfanyabiashara wa nguo mkazi wa  kijiji cha Magongomoka mkoa wa Singida, Shija Kanda(30),ameibiwa  shilingi  milioni moja na laki nane baada ya kupewa karanga  kwenye basi (jina linahifadhiwa)na kujikuta  hajitambui tena baada ya kutumia karanga hizo.


Tukio hilo la aina yake limetokea juzi huku mfanyabiashara huyo akitajwa kuwa miongoni mwa watu wengi ambao wameathiriwa na wimbi wizi wa kutumia madawa ya kulevya kwa wasafiri wanaotumia  mabasi.

Hivi karibuni umeibuka wizi wa kutumia madawa ya kulevya katika mkoa wa Shinyanga  ambapo watu kadhaa wamekuwa wakiibiwa mamilioni ya fedha baada ya kupewa pipi,juisi na karanga zilizowekewa madawa hayo.


Akisimulia mkasa huo katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga alikolazwa wodi namba mbili kitanda namba tano,Shija alisema mkasa huo ulimpata akiwa kwenye basi hilo akitoka Singida kwenda mkoani Mwanza.

Alisema alipewa karanga na mtu  aliyekuwa amekaa karibu naye aliyejitambulisha kwamba alikuwa anaelekea Kahama.


Alisema baada ya kutumia karanga hizo hakujitambua tena lakini baada ya kufikishwa hospitali na kuwekewa dripu ya maji ndipo alikuja kubaini kuwa fedha zote alizokuwa amebeba kwa ajili ya kwenda Mwanza kununua nguo za biashara zimeibiwa zote pamoja na simu yake.

“Nilikaa kwenye basi na mtu huyo tukielekea mkoani Mwanza kwenda kununua nguo za biashara,lakini nimeibiwa kwa kula karanga” alieleza Shija

Shija aliyeonekana kuchanganyikiwa  huku nguo zake zikiwa  na matapishi ambazo zilionekana kuchanwa chanwa mifuko yake,aliwataka wasafiri kuwa makini wanaposafiri na kuepuka mazoea na watu wasiowafahamu.


Muuguzi wa zamu wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga,Beas Moyo alikiri mfanyabiashara huyo kufika hospitali hiyo akiwa hajitambui na kuwekewa dripu ya maji na kwamba matukio ya kupewa madawa ya kulevya wasafiri yamekithiri mkoani Shinyanga hivyo ni vyema wananchi wakawa makini.

“Kuna watu kama watano waliwahi kuletwa hapa wakiwa wamenyweshwa madawa ya kulevya wengine walipewa pipi,juisi na tulishawahi kupokea mzungu mmoja ambaye naye alikuwa amenyweshwa madawa hayo na  wote walikuwa wameibiwa fedha na mali zao nyingine” aliongeza muuguzi huyo.
Alizitaja barabara zilizokithiri kwa wasafiri  kupewa madawa ya kulevya kuwa ni kutoka Dodoma  hadi Mwanza na Kahama hadi Musoma na kwamba baadhi ya  stendi za mabasi zina watu wanaotoa madawa ya kulevya kwa wasafiri kwa kuwauzia juisi na pipi.
“Kuna kijana mmoja alikuwa anatoka kahama alipewa juisi stendi ya  Ibinzamata maarufu kwa jina la Manyoni mjini Shinyanga baada ya kunywa hakujitambua tena na aliibiwa fedha shilingi milioni nane” alisema muuguzi huyo.

No comments:

Post a Comment