Wednesday, September 24, 2014

MAJAMBAZI YAVAMIA MADUKA NA OFISI YA KUKATA TIKETI KISHA KUPORA NA KUUWA MTU MMOJA

WATU wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wanatuhumiwa kumuuwa mtu mwenye umri kati ya miaka 35 na 40 ambaye jina lake halikuweza kufahamika na kumjeruhi mwingine. 
Tukio hilo lilifanyika kwenye maduka yaliyopo kwenye Stendi Kuu ya Maili Moja wilayani Kibaha, jirani na kituo cha Polisi baada ya watu hao kufanya tukio la uhalifu.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani lipo katika msako mkali wa watu hao waliovamia duka liitwalo Bahati, mali ya Hashim Kisaka wakiwa na bunduki na pia walivamia ofisi ya kukata tiketi ya mabasi yaendayo mikoani kisha kupora fedha kwenye maduka hayo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Athumani Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 2 kasoro usiku Septemba 20 mwaka huu.
“Watu hao walivamia katika maeneo hayo wakiwa na silaha ambayo bado haijafahamika na kumuua mtu huyo kwa kumpiga na risasi ya kifuani kisha kumjeruhi mguuni mfanyabiashara wa korosho Ambwene Mwambungu wakati wa tukio hilo ambalo lilifanyika huku umeme ukiwa umekatika na hali iliyofanya kukawa na giza nene na watu hao kutumia mwanya huo kutekeleza tukio hilo,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alieleza kuwa, kwenye tukio hilo watu hao wakiwa na silaha hiyo walivamia katika maduka hayo na kuanza kupiga risasi hewani hali iliyowafanya watu waliokuwa katika eneo hilo kukimbia hovyo huku wakiacha mali zao kuhofia usalama wao, kisha kupora fedha na mali ambayo thamani yake bado haijafahamika.
“Marehemu alifikwa na mauti wakati akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi huku majeruhi wa tukio hilo bado amelazwa akipatiwa matibabu kutokana na majeraha ya mguu aliyoyapata,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja kutoa taarifa mara moja watakapobaini walipo watu hao pia kutoa taarifa mara wanapohisi watu wasioeleweka katika maeneo yao.
 
 Via: Eddy Bog

No comments:

Post a Comment