Thursday, September 4, 2014

WALIMU WAGEUKA MADEREVA BODABODA SAA ZA KAZI NA KUSABABISHA UFAULU WA WANAFUNZI KUSHUKA

Mbunge wa Sengerema (CCM),William Ngeleja.
 
Walimu wa Shule za Msingi katika Kata ya Buzirasoga, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza, wanadaiwa kugeuka madereva wa pikipiki, maarufu kama “Bodaboda” wakati wa saa za kazi na kusababisha kata hiyo kuwa ya mwisho kwa ufaulu wa matok
eo ya mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013.

Malalamiko dhidi ya walimu hao yamedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi na yametolewa katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, uliofanyika katika Kijiji cha Ikoni, hivi karibuni.


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buziarasoga, Alfonsi Bondo, alitoa malalamiko hayo mbele ya Ngeleja na kuomba walimu wanaohusika na biashara hiyo wawajibishwe, kutokana na kuchangia kushuka kwa ufaulu wa mitihani ya taifa.

Alisema kero hiyo imekuwapo kwa muda mrefu na tayari ilishazungumziwa katika baadhi ya vikao vya kwa ngazi ya kijiji na kata, lakini kutokana na kuwapo mazingira ya kulindana, hakuna hatua zilizochukuliwa na badala yake wadau wanaofuatilia wamechukuliwa kama maadui wa walimu hao.


Akijibu malalamiko hayo, Ngeleja alisema tuhuma hizo zinawagusa watumishi wa umma, hivyo kwa mujibu wa sheria, malalamiko yao yanapaswa kuzingatia mkondo wa uwasilishaji ili yafanyiwe kazi na akamtaka Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Eliza Amos, kulitolea taarifa kwa maandishi.

Akijibu tuhuma hizo kwa niaba ya walimu wenzake wa kata hiyo, wiki iliyopita, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bazirasoga, Moshi Paulo, alisema walimu wamekuwa wanatumia pikipiki hizo kwa shughuli zao binafsi na matumizi ya bodaboda huzitumia wakati usio wa kazi.

“Kwa mfano, katika shule yangu kuna walimu wanane wanaomiliki pikipiki baadhi wamekuwa wanazitumia kwa shughuli zao binafsi na huzitumia kwa biashara, ikiwamo usafirishaji abiria wakati wa wikiendi, mapumziko na likizo, lakini siyo wakati wa saa za kazi,” alisema Paulo.

Akizungumzia madai ya utoro na kutoishi katika vituo vya kazi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Isome, Masele Gelema, alithibitisha baadhi ya familia zao kuishi nje ya vituo vyao vya kazi kutokana na shule kutokuwa na nyumba.

Katika taarifa yake, Mratibu wa Elimu Kata ya Buzisoga, Robert Cheyo, alithibitisha kuwapo kwa madai hayo na tayari yanafanyiwa kazi, lakini akiwatetea kwa madai tuhuma hizo zimetiwa chumvi.

Afisa Elimu Wilaya ya Sengerema, Juma Mwanjombe, alithibitisha kupokea madai hayo, lakini akasema ni mapema mno kuelezea matokeo ya tuhuma hizo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment