Monday, July 21, 2014

WAUMBUKA BAADA YA KUWATOZA PESA WAJAWAZITO NA WATOTO HUKO GEITA NI KATIKA KITUO KIMOJA CHA AFYA.

 

Watumishi  wawili  wa   idara  ya  Afya  katika kituo  cha Afya  cha Katoro  Wilayani Geita  Mkoani  Geita  wamekumbwa  na  kashfa baada  ya kudaiwa  kuwatoza fedha   wanawake  wajawazito  pamoja  na watoto wadogo kwa  ajili  ya matibabu  kinyume cha sheria  na sera ya  afya  inavyoelekeza .
Watumishi   hao ni  Janeth Ayoub na Hilda Cosmas ambao wanadaiwa  kuwatoza  wanawake  wajawazito  na watoto kwa  nyakati tofauti  wakati wakiwa  katika wodi ya  wazazi  ya  kituo hicho.
Wanawake waliotozwa fedha ni bi Tatu  Juma, Witness Majaliwa na  Schola  Clement.

 Wakitoa  malalamiko yao mwishoni mwa wiki  iliyopita kwa  diwani wa Kata ya  Katoro  Gervas  Daud  Kabulu walisema walifika   katika kituo hicho Julai  14 mwaka  huu  na kutozwa  kiasi  cha shilingi  elfu kumi na tano( 15,000/=) kwa  ajili ya  matibabu  kwa  kila mmoja  na shilingi elfu nane(8,000  kwa   ajili ya  ununuzi wa mipira (gloves).

Mmoja  kati  ya wanawake  hao Bi Schola  alisema kuwa alitozwa  kiasi cha Tsh  15,000  kwa ajili ya  kugharamia matibabu ya  mwanae  mchanga  Asteria  Kabodeko  wa umri wa wiki mbili(2) ambaye alikuwa  amelazwa  katika kituo hicho .
Wengine waliodai kutozwa pesa ni bi  Lydia  Nuhu na  Rehema   Elias   ambao  walilazimika kutoa shilingi 23,000/=  na   watumishi  hao waliokuwa  zamu  katika  wodi  ya  wazazi usiku wa kuamkia Julai 16  mwaka huu  .
Bi Lydia  alisema   alifika  katika kituo hicho majira ya  saa 9 usiku wa kuamkia Julai 16  katika  kituo  hicho  na kupokelewa  na  watumishi hao  waliokuwa  zamu   akiwa  na  mjamzito Neema Elikana  na kumpeleka   katika   wodi  ya wazazi ambapo baada kufikishwa  ndani  ya  wodi aliombwa  shilingi  elfu  nane (8,000)  kwa ajili ya kununua mpira (gloves).

Aliongeza kuwa   kulipokucha   alfajiri Julai 16  alitozwa  elfu  15  baada  ya  Neema  kumaliza kujifungua  na kupoteza   fahamu .
Lydia  alisema  baada  ya Neema  kupoteza  fahamu aliombwa  fedha hiyo ili  mgonjwa wake aongezewe  maji (Dripu)  kwa madai kuwa  katika kituo hicho  maji  hayapo  na stoo  ya  dawa imefungwa  hivyo alilazimika  kutoa  fedha hiyo ili   kunusuru  maisha  ya mtoto wake.

Kufuatia   malalamiko  hayo  diwani wa kata  hiyo aliamua kumuita   Mganga  Mkuu wa  kituo  hicho  Dk  Alex  Gatuku  na kumweleza  malalamiko hayo  ambapo alionyesha kushangazwa  na hali hiyo na   kuamua kuorodhesha  majina  ya wanawake wanane (8)  waliodai kutozwa  fedha  wakiwemo  wazazi  waliojifungua ndani  ya siku saba ambao pia walikiri   kutozwa fedha  na  mtumishi wa wakiume ambaye  jina lake hali kufahamika  mara moja .
Naye mganga  mkuu akalazimika  kuwaita  watumishi  wawili waliokuwa  zamu  usiku wakuamkia  Julai 16  katika wodi  hiyo   na kufanya  nao kikao cha  dharura  mbele  ya  diwani wa kata hiyo  na katibu mwenezi  wa  chama  NCCR Mageuzi  jimbo   la Busanda Justin Girobi ambae waliambatana na diwani huyo.

 Watumishi  hao walikiri  kuwatoza   fedha  kiasi  cha 23,000 elfu  kutoka  kwa   Bi Lyidia   na  elfu  nane  (8,000)  kutoka  kwa  Josephine   James  na  hivyo  kuamriwa  kuzirejesha  kwa  akina mama  hao waliokuwa  ndani ya  kikao hicho.
Watumishi hao  walipotakiwa  kueleza  sababu  ya  kuwatoza  fedha  akinamama  hao  walisema lengo lilikuwa ni kutaka  kuwasadia  kwa kuwa mtunza funguo  katika stoo  ya dawa  anakaa mbali  na kituo  na kwamba  utaratibu  wa  kuwataka waja wazito kuja  na  glove  na  kapeti upo katika kituo hicho wala siyo utaratibu mpya. 

“Tuliamua  kumueleza  ndugu   wa mgonjwa   Bi Lydia  tukaenda  kununua  kwa  mlinzi wa kituo  hiki  Magoti  Kahitila  usiku huo  kwa kuwa ndiye  huwa anatuuzia  inapohitajika",walisema.

Hata hivyo  utetezi  huo ulipingwa  vikali na Mganga mkuu wa kituo  hicho .
 "Nasema  ni  marufuku  kuuza   gloves   katika eneo hili  na  kuwatoza  fedha  wajawzito  na watoto  ni talia  na nyinyi  kwanza  kabla  Mganga mkuu wa  Wilaya (D M O )   hajaja,",alisema    Gatuku  kwa  msisitizo.
  

    mganga mkuu  wa wilaya  ya   Geita ( D M O ) Dk  Noel  Makuza na  alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alisema.....

 "Nimesikitishwa  na  hali hiyo   na nimepata  taarifa hiyo jana  kutoka  kwa  diwani  wa kata    hiyo  na  kwamba  nimeanza  kuchukua  hatua  na watakaobainika  sheria ya  itachukuwa  mkondo  wake’’.
"Asante  kwa kunipa  taarifa  mwandishi  najua inauma  akina  mama  na watoto  wadogo  kutozwa  fedha , si utaratibu wetu, lengo letu  ni  kuboresha utoaji wa huduma  kwa  jamii  na tayari nimeshatoa   maelekezo kwa uongozi wa  kituo hicho  kuhusiana na tatizo hilo''.

Na Valence Robert.

No comments:

Post a Comment